KWA mtazamo wa haraka katika programu za kwanza
za mazoezi ya kocha mpya wa Yanga,Hans van der Pluijm ni kwamba
kutatokea mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha kwanza.
Kocha huyu mpya raia wa Uholanzi alianza mazoezi
juzi Jumamosi, si muumini wa soka la kujilinda bila kushambulia na
anapenda kazi ya kuzuia ifanywe na kila mchezaji wake kikosini bila
kujali nafasi achezayo.
Hii ni mara ya pili kwa Pluijm kupewa jukumu la
kuifundisha Yanga baada ya awali kupewa kazi hiyo akichukua mikoba ya
Ernie Brandts ambaye aliachishwa kazi na timu hiyo baada ya kupoteza
mchezo wa Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba mwaka jana.
Kabla ya ujio wake, Yanga ikiwa chini ya Kocha
Marcio Maximo imekuwa ikicheza soka la kujilinda na kujikuta
ikitengeneza nafasi chache za kufunga, na hata ikipata ushindi huwa wa
mabao kiduchu. Yafuatayo ni mabadiliko yatakayofanywa na Pluijm katika
kusuka muziki mpya wa Yanga;
Mbuyu Twite arudi kulia
Kwa sasa Mbuyu Twite anacheza kiungo mkabaji
lakini wakati wa Pluijm alikuwa anacheza beki ya kulia ambapo alikuwa
anacheza huku akipandisha mashambulizi ya timu yake na kuzuia wakati
huohuo. Huko Twite huwajibika ipasavyo katika kuzuia mashambulizi ya
mawinga wasumbufu kama Emmanuel Okwi na Deus Kaseke wa Mbeya City. Beki
wa sasa wa kulia wa Yanga, Juma Abdul hataweza kuwa na nafasi ya kucheza
katika kikosi cha sasa kwani kitendo chake cha kupandisha timu na
kuchelewa kurudi katika nafasi yake kitamgharimu na anatakiwa kufanya
kazi ya ziada kuhakikisha anarudisha imani kwa kocha wake. Ikitokea
Twite akiwa majeruhi au vinginevyo basi Salum Telela atacheza beki ya
kulia kwani ana uwezo wa kuzuia na kupandisha timu.
Hassan Dilunga kurudi kikosini
Hadi katika mechi ya mwisho ya Maximo dhidi ya
Simba, kiungo Hassan Dilunga alikuwa benchi kwani hakuendana na mfumo
wake wa kuzuia kwa muda wote bila kuipeleka mbele timu. Maximo alitoa
nafasi kwa Twite na Emerson Roque kucheza nafasi hiyo lakini alilazimika
kumuingiza Dilunga dakika ya 45 baada ya Twite kuumia. Pluijm hata
kabla hajaondoka alikuwa anamuamini kuwa kiungo mzuri na alimtumia
katika mechi kadhaa akicheza kwa kuzuia na kushambulia japokuwa si mzuri
sana kwenye kuzuia. Taratibu Dilunga atarejea kikosini lakini kiungo
Said Juma ‘Makapu’ ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuanza kwani ni mzuri
katika kuzuia na kupandisha timu na tayari Pluijm anamuandaa ili
achezea dhidi ya Azam FC Desemba 28, mwaka huu. Makapu alifanya vizuri
katika mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Azam ambayo Yanga ilishinda
mabao 3-0 na kocha ameshapewa taarifa hizo hivyo anapanga kumrejesha
katika nafasi hiyo huku msaidizi wake akiwa Dilunga. Hivyo, Makapu
ataanza na kama mambo hayataenda vizuri basi Dilunga ataingia kuchukua
nafasi yake ili kuokoa jahazi. Maximo hakuendelea kumpa nafasi Makapu
licha ya kucheza vizuri dhidi ya Azam.
Kaseja benchi
Ingawa bado anavutana na viongozi wa Yanga, lakini
kuna uwezekano mkubwa wa kipa Juma Kaseja kuanza mazoezi ya kuichezea
Yanga na kurejeshwa moja kwa moja katika kikosi cha timu hiyo akimsaidia
kipa namba moja Deo Munishi ‘Dida’ kwani tangu zamani Pluijm alimfanya
Kaseja kuwa msaidizi wa Dida. Hii inamaanisha kwamba, Ally Mustapha
‘Barthez’ ambaye sasa ni namba mbili huenda akalikumbuka dirisha dogo
kwani ataondoka benchi na kusubiri jukwaani endapo Kaseja atakuwa katika
ubora wake. Pluijm anapanga kumrudisha Kaseja uwanjani licha ya kipa
huyo kutotokea katika mazoezi ya Yanga tangu ligi iliposimama na
hakushiriki maandalizi ya mechi ya Nani Mtaji Jembe.
Salum Telela katikati
Kiungo Salum Telela anaweza kuwa mmoja wa
wachezaji wa Yanga wanaofurahia kurejea kwa Pluijm kwani ni kipenzi cha
kocha huyo raia wa Uholanzi. Pluijm anapanga kumchezesha Telela kiungo
namba sita na kama ikitokea mambo yakiharibika kwa Twite basi kiungo
huyu atacheza namba mbili yaani beki wa kulia kwani anamudu kucheza
nafasi hiyo. Kwa sasa Telela anaonekana yupo fiti baada ya kusumbuliwa
na majeraha ya muda mrefu hivyo kuwa mtu wa benchi japokuwa ana uwezo
mkubwa wa kucheza soka. Hata hivyo kwa sasa ataanza Makapu kutokana na
uwezo wake kuonekana kumvutia kocha kutokana na kufanya vizuri dhidi ya
Azam katika mechi ya Ngao ya Hisani.
Mwanaspoti
Mwanaspoti
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni