KAMA Simba hii ikikamilika mmekwisha. Kocha wa
Simba, Patrick Phiri ameutaka uongozi wa klabu hiyo kufanya usajili wa
wachezaji sita wenye uwezo wa juu huku straika wa Mtibwa Sugar, Ame Ally
na beki Hamis Kessy wakiwa chaguo lake la kwanza, Mwanaspoti
linafahamu.
Mbali na mastaa hao wa Mtibwa,uongozi umetangaza
kumnunua winga wa Yanga, Simon Msuva. Phiri alisema endapo uongozi
utampa nafasi ya kupendekeza usajili wa wachezaji wa kigeni atawaletea
mastaa wa maana kutoka Zambia.
Phiri aliingia matatani kwenye kikosi hicho baada
ya Simba kucheza mechi sita bila kupata ushindi jambo ambalo amesema
hataki litokee tena Msimbazi. Simba ilishinda mchezo mmoja pekee katika
mechi saba za msimu huu na kutoka sare mara sita.
Kocha huyo alitumia muda wa siku mbili akiwa
amejifungia kwenye moja ya nyumba tulivu eneo la Kunduchi, Dar es
Salaam kuandaa ripoti ya mechi saba za msimu huu na kutoa mapendekezo
kadhaa ya marekebisho na kuikabidhi kwa viongozi juzi Jumatano mchana na
jana Alhamisi alitarajia kukutana na viongozi wake kwa ajili ya
kuijadili.
Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Zambia
‘Chipolopolo’, alisema anahitaji winga mmoja, kiungo mchezeshaji mmoja
na straika wa kati mmoja ili kuifanya safu yake ya ushambuliaji kuwa ya
kutisha zaidi nchini.
Imefahamika kuwa licha ya kocha huyo kuruhusiwa
kupendekeza wachezaji kutoka Yanga na Azam, ameelekeza nguvu kubwa
kuwanasa mastaa kadhaa kutoka kwenye kikosi cha Mtibwa wakiwemo straika
Ame na Kessy.
“Nataka kikosi kifanyiwe marekebisho kadhaa
hususani kwenye eneo la beki na ushambuliaji. Kwa kifupi ni kwamba
nahitaji winga wa kulia mmoja, kiungo mchezeshaji mmoja na straika wa
kati mmoja, nahitaji pia beki wa kulia mmoja na beki wa kati mmoja,”
alisema Phiri na kubainisha kuwa anahitaji wachezaji sita pekee.
“Kuna wachezaji wawili wa Mtibwa nimewapendekeza,
sema siwafahamu majina hivyo nimeandika namba zao, kuhusu wachezaji
kutoka nje nimeliacha hilo kwa viongozi lakini kama wataniruhusu naweza
kuja na wachezaji wazuri kutoka Zambia,” anaeleza Phiri na kusema kuwa
atakwenda kwao kwa mapumziko mwishoni mwa wiki hii.
Akieleza sababu za kuwapiga chini mastaa wa Yanga
kwenye mapendekezo yake hayo, Phiri alisema bado hajaona mchezaji wa
klabu hiyo mwenye kiwango cha juu wa kuweza kuisaidia Simba msimu huu
hivyo ni vyema akasajili kutoka kwenye klabu nyingine ingawa tayari
waajiri wake wametangaza rasmi kufukuzia saini ya Simon Msuva.
Taarifa za ndani kutoka Simba pia zinaeleza kuwa
kuna uwezekano wa klabu hiyo kumrejesha beki Shomary Kapombe, ambaye
yuko Azam lakini kwa makubaliano ya kubadilishana na mmoja wa mastraika
wa timu hiyo jambo ambalo bado linajadiliwa.
Wakati huo huo, Phiri alisema anafahamu kuwa
amebakisha mtihani mmoja ili aweze kuendelea na kibarua chake Simba na
kuutaja mtihani huo kuwa ni kuifunga Yanga kwenye mechi ya Nani Mtani
Jembe, Desemba mwaka huu.
“Nafahamu kilichompata kocha wa Yanga (Ernest
Brandts) msimu uliopita, nahafamu kuwa alifukuzwa baada ya kufungwa
kwenye mechi hiyo, ni lazima nishinde ili kujiweka pazuri.
Mwanaspoti
Mwanaspoti
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni