YANGA wanadai wameshtukia kwamba Juma Kaseja
anamshawishi Haruna Niyonzima asajili Simba na tayari wamemchimba biti
la uhakika ingawa kiungo huyo amesisitiza kwamba hatasaini mkataba mpya
Jangwani.
Tayari, kiungo huyo anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine anayotaka kutokana na mkataba wake kubakiza miezi sita.
Katika mazungumzo yake na Mwanaspoti Niyonzima
ameeleza kushangazwa na kitendo cha kocha Marcio Maximo kumtoa kipindi
cha pili bila kuambiwa sababu ili ajirekebishe. Alitolewa kwenye mechi
nne mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya Stand United, Kagera, Simba na
Mgambo.
“Mimi ni mchezaji, ninaitumikia timu yangu ya
Taifa, pia ni tegemeo katika timu hiyo, ninacheza dakika 90, sasa iweje
hapa Yanga natolewa kipindi cha pili?” alihoji mchezaji huyo mzoefu.
“Kitu kingine kinachonichosha Yanga ni uzushi,
ule ninaosambaziwa na baadhi ya wanachama (makomandoo) kuwa Kaseja
ananishawishi nisaini Simba, kwa kuwa tunalala chumba kimoja tunapokuwa
kambini,” alisema Niyonzima.
Ishu ya Kaseja
Meneja wa Kaseja, Abdulfatah Saleh amesema
mchezaji huyo ni huru na anaweza kujiunga na Simba muda wowote kuanzia
sasa kwani vitendo alivyofanyiwa na Yanga ni kama kuvunjiwa mkataba.
Abdulfatah aliliambia Mwanaspoti; “Ni kama Kaseja
hana mkataba na Yanga kwani kila kitu kinajieleza katika mkataba wake
ikiwemo kumaliziwa fedha yake na nafasi ya kucheza, sasa Yanga
haijatimiza vitu vyote hivyo.
“Mteja wangu yupo huru kwani Yanga kwa kutotimiza
hayo mambo wamevunja mkataba na kama kuna kiongozi wa Yanga anasema
hawadaiwi na Kaseja ajitokeze, haiwezekani watu wakiuke makubaliano
kienyeji.”
Kuhusu Simba kuwa na nia ya kumsajili Kaseja,
Abdulfatah alisema; “Nimesikia Simba wanamtaka Kaseja, hiyo haina tatizo
kwani wameonyesha nia ya kumchukua kwa sababu wanafahamu kuhusu uwezo
wake waje tuzungumze tufanye biashara.” Lakini Mwanaspoti linajua kwamba
kipa huyo ameshafanya mazungumzo na kumalizana na Simba na kuanzia
Januari atakuwa kwenye uzi wa Simba.
Tangu aliposajiliwa na Yanga Novemba mwaka jana,
Kaseja ameshindwa kupata nafasi kikosi cha kwanza na kutoa nafasi kwa
Deo Munishi ‘Dida’ katika mechi nyingi za Ligi Kuu Bara hata za
kirafiki.
Mwanaspoti
Mwanaspoti
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni