Azam kupiga kambi mara mbili
Azam FC wanatarajia kuwa vipindi viwili vya maandalizi kwa ajili ya msimu mpya unaokuja wa 2015/16
WASHINDI wa pili wa Ligi ya Vodacom msimu uliopita Azam FC, wanatarajia kuwa vipindi viwili vya maandalizi kwa ajili ya msimu mpya unaokuja wa 2015/16.
Mtendaji mkuu wa klabu ya Azam FC Saad Kawemba, ameiambia Goal sehemu ya kwanza itakuwa ni michuano ya Kombe la Kagame ambayo inatarajia kuanza Julai 11 Jijini Dar es Salaam na baada ya kuisha michuano hiyo watatoka nje ya nchi kwenda kupiga kambi ya mwezi mmoja ambayo itawaweka tayari kwa ajili ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi ya Vodacom.
“Hiyo ni ratiba ambayo ameitoa kocha wetu Stewart Hall, baada ya leo kumtambulisha kwa wachezaji pamoja na jopo zima la benchi la ufundi na wataalamu wa utawala waliofika nchini kwa ajili ya kuiongoza klabu yetu,”alisema Kawemba.
Hall anayerejea Azam kwa mara ya tatu ameanza mazoezi na wachezaji wachache na amesema kazi yake kubwa atakayo anza nayo ni kujenga akili za wachezaji wake kabla ya kutimia kwa wachezaji waliopo kwenye timu za taifa na kuanza program maalumu kujiandaa na msimu ujao.