Vatican, Italia. Kiongozi wa
Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis kwa mara ya kwanza ametabiri
hatima ya maisha yake duniani akisema kuwa anaamini Mungu anaweza kumpa
muda wa miaka miwili au mitatu ya kuishi.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ndege
wakati akitoka ziarani Korea Kusini kurejea Vatican, Papa Francis
alisema suala la kuendelea kuishi ni neema ya Mungu.
“Suala hili naliona kama neema tu ya Mungu kwa
watu wake. Najaribu kutafakari kuhusu dhambi zangu na makosa yangu,
siwezi kujivuna. Najua kwa sababu hali hii itadumu kwa muda mchache.
Miaka miwili au mitatu nitakuwa nimeondoka na kwenda nyumbani kwa baba,”
alisema.
Papa Francis (77), pia alizungumzia uwezekano wa kustaafu endapo atahisi kwamba afya yake hairuhusu kuendelea na kazi.
Utamaduni wa kuachia madaraka ndani ya kanisa hilo
linalotajwa kuwa na waumini wengi duniani uliasisiwa upya mwaka jana na
mtangulizi wake, Papa Benedict XVI aliyeng’atuka kutokana na matatizo
ya kiafya.
Pamoja na kwamba Papa Francis hajawahi kuzungumza
hadharani kuhusu ni lini pengine anaweza kufariki dunia, lakini baadhi
ya vyanzo vya habari kutoka Vatican vinasema kuwa kiongozi huyo amekuwa
akiwaambia watu wake wa karibu kuhusu siku zake chache zilizosalia
duniani.
Wachambuzi wa masuala ya kiimani kwa nyakati tofauti walisema huenda kiongozi huyo ana tatizo la kiafya ambalo halijawekwa wazi.
Wakati hayo yakiendelea taarifa za ndani
zinabainisha kwamba kiongozi huyo aliwahi kutolewa pafu moja baada ya
kuathirika wakati akiwa kijana nchini Argentina.
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni