TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - RELEASE NO. 97
TAREHE 13 JUNI, 2015
STARS YAWASILI BORG EL ARAB, KUWAVAA MISRI KESHO
Msafara
wa timu ya Taifa ya Tanzania (taifa Stars) inayodhaminiwa na kampuni ya
bia ya Kilimanjaro Premium Lager tayari umewasili salama katika eneo la
Borg El Arab jijini Alexandria na kufikia katika hoteli ya Panacea
tayari kwa mchezo wake wa kesho.
Taifa Stars ambayo ilikuwa kambini nchini Ethiopia kwa takribani
wiki moja, iliondoka jana usiku Addis Ababa na kuwasili uwanja wa ndege
wa Cairo majira ya saa 8 usiku, kisha kuunganisha kwa usafiri wa basi
mpaka Borg El Arab takribani masaa matatu.
Kocha mkuu wa Taifa Stars Mart Nooij, atakiongoza kikosi chake
katika mazoezi ya mwisho leo saa 1 usiku katika uwanja wa Borg El Arab
kwa saa za Misri, sawa na saa 2 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Akiongelea mchezo wa kesho, Nooij amesema anashukuru kikosi
kimefika salama nchini Misri na kipo katika hali nzuri, vijana wana ari
na morali ya hali ya juu, anaamini kesho timu itfanya vizuri katika
mchezo huo dhidi ya wenyeji Misri.
Nooij amesema mchezo wa kesho ni muhimu kwake, na kikosi chake
kitacheza mpira wa kasi na pasi za haraka haraka, huku safu ya
ushambuliaji ikihakikisha inatumia vizuri nafasi itakazozipata.
Aidha kuelekea katika mchezo huo wa kesho, kiungo Amri Kiemba
ameungana na wachezaji wengine waliokuwa kambini Addis Ababa kuchukua
nafasi ya Mrisho Ngasa ambaye alishindwa kuungana na timu kutokana na
sababu zilizopo nje ya uwezo wake.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia
tayari amewasili jijini Alexandria kwa ajili ya kuipa sapoti Taifa Stars
katika mchezo huo wa kesho.
Mchezo kati ya Misri na Tanzania utachezwa kesho saa 2 usiku kwa
saa za Afrika Mashariki na kati katika uwanja wa jeshi la Misri (Borg El
Arab) uliopo takribani kilometa 70 kutoka jijini Alexandria na kilometa
200 kutoka jiji la Cairo.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni