LOGO

Kocha wa Simba Patrick Phiri

Kocha wa Simba Patrick Phiri amesema atawatumia kwa pamoja washambuliaji wake hatari watatu Emmanuel Okwi, Raphael Kiongera na Amis Tambwe kwenye mchezo wa kesho wa ufunguzi wa ligi kuu ya Bara dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa. Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu toka Zanzibar, Phiri ambaye anaiongoza Simba kwa awamu ya tatu kwenye ligi kuu ya Bara alisema amepanga kuwaanzisha washambuliaji hao kwenye mfumo wa 4-3-3 lengo likiwa ni kutengeneza nafasi nyingi za kufunga na kuzitumia. "Tumefanya mazoezi leo (jana) asubuhi na kuna maendeleo makubwa... nimefanyia kazi mapungufu kwenye safu yangu ya ushambuliaji mambo safi," alisema Phiri. Alisema kuwa kikosi chake kipo katika hali nzuri na wanategemea kufika jijini Dar es Salaam leo au kesho asubuhi tayari kwa ajili ya kuwakabili 'Wagosi wa Kaya' kwenye mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu. "Coastal ni timu nzuri. Binafsi sijawaona lakini naamini ni timu yenye ushindani," alisema Phiri."Kikosi changu kitacheza kwa tahadhari kuhakikisha tunapata ushindi na kuanza vizuri ligi." Phiri aliiongoza Simba kutwaa ubingwa wa Bara misimu mitano iliyopita kwa kucheza mechi zote 26 bila kufungwa. Alisema katika mchezo wa kesho atawakosa beki wa pembeni Issa Rashid 'Baba Ubaya' ambaye ana maumivu ya nyama za paja na kiungo Jonas Mkude aliumia goti. Wakati huo huo, kocha wa Coastal Union Yusuph Chippo amewapa mtihani wachezaji wake kuhakikisha wanapambana kufa na kupona ili kuchukua pointi tatu dhidi ya Simba kesho.
 

NIPASHE

0 comments Blogger 0 Facebook

Chapisha Maoni

ZILIZOSOMWA SANA

 
TASWIRA MICHEZONI © 2015. All Rights Reserved. This Blog Proudly Designed by MMC™ Media Group Ltd | Phone +255-786-758-021
Top