LOGO

Kocha Mkuu wa Yanga,Mbrazil Marcio Maximo

Kocha Mkuu wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo ameawaomba radhi wanachama na mashabiki wa Yanga baada ya timu yake kuanza vibaya msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
Kikianza na wachezaji wanne wa kimataifa, Wanyaruanda Haruna Nyinzoma na Mbuyu Twite, Mganda Hamis Kizza na Mbrazil Genilson Santos Santana ‘Jaja’, Kikosi cha Yanga kilijikuta kikikubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya timu isiyo na mchezaji hata mmoja wa kimataifa, Mtibwa Sugar katika mechi yao ya kwanza ya VPL msimu huu iliyopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Maximo, kocha wa zamani wa timu ya Taifa (Taifa Stars) amelazimika kuwaomba radhi Wanajangwani kutokana na kipigo hicho huku akiahidi kufanya vizuri katika mechi zinazofuata.
“Maximo anawaomba radhi wapenzi, mashabiki na wanachama wa Young Africans (Yanga) waliojitokeza kwa wingi mjini Morogoro kushangilia timu yao kwa matokeo mabaya ya kupoteza mchezo wa kwanza.
Ameahidi kuhakikisha kuwa timu inajipanga vizuri ili kupata pointi zote tatu katika mechi inayofuata,” inasomeka sehemu ya taarifa ya uongozi wa Yanga iliyowekwa kwenye mtandao wa klabu hiyo.
Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa Maximo amesema amekubaliana na matokeo, lakini hakuridhishwa na maamuzi ya marefa wa mechi hiyo.
Lakini, Kanuni za Ligi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) haziruhusu makocha kutoa maoni kuhusu uchezeshaji wa marefa wa mechi husika.
Mabao ya Mtibwa katika mechi hiyo iliyoshuhudiwa mshambuliaji mpya wa Yanga kutoka Brazil Jaja akikosa penalti mwanzoni mwa kipindi cha pili, yalifungwa na mchezaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi na Ame Ali aliyekuwa mwiba mkali kwa Yanga siku hiyo.
Kipigo hicho ni mwendelezo wa ‘uteja wa Yanga kwa Mtibwa’ kwani Yanga haijawahi kuwafunga mabingwa hao wa 1999 na 2000 wa Tanzania Bara kwenye uwanja huo tangu Septemba 19, 2009 Wanajangwani waliposhinda 2-1, mabao yakifungwa na Mrisho Ngasa na Nurdin Bakari.
Kikosi cha Yanga, ambacho kinatiwa nguvu na kupona kwa kiungo mpya kutoka Brazil Andrey Coutinho, kinaendelea na mazoezi jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi inayofuata.

0 comments Blogger 0 Facebook

Chapisha Maoni

ZILIZOSOMWA SANA

 
TASWIRA MICHEZONI © 2015. All Rights Reserved. This Blog Proudly Designed by MMC™ Media Group Ltd | Phone +255-786-758-021
Top