KOCHA mpya wa Simba, Patrick Phiri amesema ameamua kuja
kukinoa kikosi hicho huku akiamini kikubwa kilichomleta hapa nchini ni mapenzi.
Phiri raia wa Zambia kwa mara ya kwanza amefanya
mahojiano mara baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuinoa Simba na kusema
urafiki wake na watu wengi waliopo Simba, umemfanya aache ofa kubwa zaidi.
“Wakati Simba wananipigia simu, tayari Namibia walikuwa
wamenitumia tiketi ya ndege kwenda Windhoek kwa ajili ya mazungumzo. Viongozi
walisafiri na timu na wakaniambia ndani ya siku chache watakuwa wamerejea,
hivyo nisafiri watanikuta huko ili tumalizie na kusaini mkataba.
“Wakati najiandaa, Simba walianza mazungumzo na mimi
baada ya kunipigia simu. Kweli lilikuwa ni jambo la kuchanganya kwangu kwa kuwa
imekuwa ni vigumu sana kusema hapana kila ninaposikia ni Simba ndiyo
wananihitaji.
“Nina mapenzi ya juu sana na Simba kwa kuwa najua watu
wa hapa (Simba) wananipenda, wananiheshimu na kunijali. Hivyo
nikachanganyikiwa, sikujua hasa sahihi ni kipi ingawa kama ni maslahi, Namibia
yatakuwa juu.
“Mwisho mapenzi yangu kwa Simba ndiyo yalinifanya
kuchukua uamuzi huu, nikasema nitakuja Dar es Salaam kuwasilikiza,” anasema
Phiri ambaye mara zote ni mtaratibu huku akisisitiza amefurahishwa zaidi kukuta
watu wengi aliowaacha wakiwepo Simba, kitu kinamfanya aamini hajakosea kuweka
mapenzi yake kwa klabu hiyo inayotumia rangi nyekundu na nyeupe.
Nitaanza kazi rasmi nikiwa Zanzibar ingawa hapa (Dar es
Salaam) ninaweza kuwaona vijana kwa ajili ya kuwasalimia na kuwaona namna
walivyoanza kufanya kazi. Najua mambo yatakuwa yanakwenda vizuri na nitakutana
na kushirikiana na watu wengi ninaowafahamu.
Matola na Nyagawa wote walikuwa nahodha katika kikosi
changu ingawa ni kwa wakati tofauti. Sasa wao ni kocha msaidizi na meneja.
Ninaamini hawa ni wanangu pia ninafurahi kuwakuta bado wakiwa Simba na hii
inaonyesha mapenzi yao makubwa kwa klabu hii kama ilivyo kwangu.
Mapenzi ni silaha kubwa kwa unachokifanya. Ninaamini
kabisa kuwa na watu wanaoipenda kazi yao na kampuni wanayoitumikia, basi
itasaidia kupatikana kwa maendeleo ambayo mnayatarajia.
Kufanikiwa lazima ufanye kazi bila ya kuchoka, ukiamini
kuwa mafanikio yanakuja baadaye. Ukiwa unakipenda kitu fulani, huwezi kuchoka
hadi mafanikio yapatikane.
Kama nilivyosema awali, ninahitaji muda ingawa
ninajiamini kabisa mambo yatakuwa mazuri. Kwangu ingawa si mgeni hapa Simba,
kikazi itakuwa ni mgeni. Nimeambiwa kuna wachezaji wengi wageni na wachache
ambao nilifanya nao kazi.
Utamaduni wa Simba hauwezi kubadilika sana, najua
kutakuwa na wachezaji wazuri ambao tukipata muda wa pamoja, tutatengeneza
kikosi bora ambacho kitafanya vizuri.
Lakini lazima tukubali katika hili kuwa muda
unahitajika, lazima kuwe na uvumilivu kidogo wakati nikiwaona wachezaji, wakati
nabadilisha mifumo, halafu mafanikio yataanza kupatikana.
Phiri aliifundisha Simba kwa vipindi viwili tofauti
(2003-05) na (2008-11) na vyote amechukua makombe tofauti yakiwemo mawili ya
ubingwa Tanzania Bara. Mwaka 2005 alitwaa Kombe la Tusker. Huku akiwa na rekodi
ya mmoja wa makocha wa Simba ambao walikuwa wakiitesa Yanga.
Wachezajii aliowahi kuwafundisha mara ya mwisho ikiwa ni
mwaka 2011 alipoondoka ni Shabani Kisiga, Nassor Said ‘Chollo’ na Amri Kiemba ambao
kwa mara nyingine atafanya nao kazi tena akiwa nao katika kikosi kimoja cha
Simba.
Moja ya sifa ya Phiri ni soka la haraka-haraka na pasi
fupifupi lakini kikosi ambacho kinacheza soka la nguvu bila kuchoka na
wachezaji wengi ambao amekuwa akiwafundisha anawajenga kujiamini zaidi
uwanjani.
Phiri aliyewahi kuwa mshambuliaji wa Nkana pia timu ya
taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’ ambayo pia aliifundisha, ni kati ya makocha wenye
heshima ya juu zaidi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Bara
la Afrika.
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni