Shirikisho
la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa
Jumatano kati ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Malawi (The Flames)
kuwa ni shilingi elfu tano (5,000) katika mchezo huo wa kuwania kufuzu
kwa fainali za kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Viingilio vilivyotangazwa leo ni
kiingilio cha juu kabisa kwa mchezo huo shilingi elfu kumi (10,000) kwa
viti vya VIP B & C, huku viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani
ikiwa ni shilingi elfu tano (5,000).
Stars inayonolewa na kocha mzawa
Charles Boniface Mkwasa imeendelea kujifua katika viwanja vya Gymkhana
na uwanja wa Taifa jioni kujiandaa mchezo huo wa Jumatano dhidi ya
Malawi, huku wachezaji wakiwa wenye ari na morali ya hali ya juu
kuelekea kwenye mechi hiyo.
Wachezaji 22 wapo kambini akiwemo
mshambuliaji Mrisho Ngasa anayecheza soka la kulipwa nchini Afrika
Kusini aliyeripoti jana mchana kambini, huku wachezaji wawili Mbwana
Samata na Thomas Ulimwengu wakitarajiwa kujiunga na wenzao leo wakitokea
Lubumbashi–Congo DR.
Wakati huo huo timu ya Taifa ya
Malawi (The Flames) imewasili nchini jana saa 4 asubuhi na kufikia
katika hoteli ya De Mag iliyopo Mwanayamala, ambapo kikosi hicho leo
kimefanya mazoezi asubuhi katika uwanja wa Boko Veterani.
Waamuzi wa mchezo huo kutoka
nchini Somalia, kamisaa na mtathimin waamuzi wa wanatarajiwa kuwasili
nchini leo na kufikia katika hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay.
Mwamuzi wa kati ni Hagi Yabarow
Wiish (Somalia), akisaidiwa na Hamza Hagi Abdi (Somalia), Salah Omar
Abubakar (Somalia), mwamuzi wa akiba Bashir Olad Arab (Somalia),
mtathimini wa waamuzi Sam Essam Islam (Misri) na kamisaa wa mchezo ni
Muzambi Gladmore (Zimbabwe).
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni