Yanga wametwaa ubingwa wa Ngao ya
Jamii baada ya kuilaza timu ya Azam FC kwa mikwaju ya penati 8-7 baada
ya sare ya bila kufungana kwenye mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii
uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Azam wameshindwa kufuta uteja
kwenye kuwania ngao hiyo, ambapo tangu wameanza kupata fursa ya kuiwania
mara zote wamejikuta wakipoteza michezo yao na kuikosa ngao hiyo ambayo
inaashiria kufunguliwa rasmi kwa pazia la ligi kuu Tanzania bara.
Golikipa wa Yanga Ali Mustafa
‘Barthez’ ameibuka shujaa kwenye mchezo wa leo akifanikiwa kupangua
penati mbili za wachezaji wa Azam na kuipa ubingwa timu yake.
Ushindi wa leo kwa Yanga ni sawa
na wamelipa kisasi baada ya kiondolewa na Azam kwenye hatua ya robo
fainali ya michuano ya Kagame mwezi Julai mwaka huu kwa changamoto za
penati ambapo leo Azam nao wamepoteza mchezo wao kwa mikwaju ya penati.
Kila timu ilipata penati nne kati
ya penati tano za kwanza wakati kila timu ilipoteza penati moja kati ya
tano. Baada ya kuwa sare kwa penati 4-4, timu zote zikaanza kupigiana
penati mojamoja ili kumsaka mshindi ndipo Yanga wakapata penati nne
nyingine huku Azam wao wakikosa penati moja na Yanga akatwaa ubingwa
huo.
Kipindi cha kwanza kilimalizika
huku timu zote zikiwa sare ya bila kufungana, timu zote zilifanya
mashambulizi kadhaa wakati wa kipindi cha kwanza lakini Yanga wakiwa
wamefanya mashambulizi mengi zaidi langoni mwa Azam.
Golikipa wa Azam Aishi Manula
alifanya kazi ya ziada kuokoa mipira kadhaa langoni mwake kufuatia
mashambulizi makali yaliyofanywa na Yanga.
Kipindi cha pili kilianza kwa
kasi ambapo Yanga waliliandama lango la Azam dakika za mapema mwa
kipindi hicho lakini bado washambuliaji wake hawakuweza kufunga goli.
Mchezo wa leo inaonekana timu
zote zilikuwa zimekamia kwani mara kadhaa wachezaji walikuwa
wakifanyiana madhambi na kupelekea mwamuzi kutoa kadi za njano.
Said Juma alioneshwa kadi ya
njano kipindi cha kwanza kwa kumchezea vibaya mshambuliaji wa Azam John
Bocco ‘Adebayo’. Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alioneshwa kadi ya njano kwa
kumfanyia madhambi Bocco kipindi cha pili wakati Mbuyu Twite yeye
alioneshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Farid Mussa . Kwa upande
wa Azam kadi ya njano ilitoka kwa Erasto Nyoni baada ya kumchezea vibaya
Saimon Msuva.
Katika kipindi cha pili timu zote
zilifanya mabadiliko, Yanga walimtoa Said Juma Makapu na nafasi yake
kuchukuliwa na Haruna Niyonzima, Donald Ngoma akampisha Deus Kaseke na
Andrey Coutinho akaingia baada ya Simon Msuva kupumzishwa. Azam
walimtoa Mudathir Yahya na kumuingiza Jean Mugiraneza huku Ame Ally
‘Zungu’ akiingia kuchukua nafasi ya Frank Domayo.
Mabadiliko hayo yalizaa matunda
kwa upande wa Yanga kwani walicheza vizuri kipindi chote cha pili wakati
Azam wao wakiwa wanazuia zaidi. Kama wachezaji wa Yanga wangekuwa
makini, wangepata goli mapema kipindi cha pili lakini walipoteza nafasi
muhimu za kufunga walizozitengeneza.
Hadi mwamuzi wa mchezo huo Martin
Saanya anapuliza kipyenga cha mwisho kuumaliza mchezo huo, timu zote
zilikuwa sare ya bila kufungana na hapo ikaidi itumike changamoto ya
mikwaju ya penati ili kumpata mshindi.
Wachezaji waliofunga penati kwa
upande wa Yanga ni Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Amis Tambwe, Andrey
Coutinho, Godfrey Mwashiuya, Thaban Kamusoki, Mbuyu Twite na Kelvin
Yondani huku penati ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ikipanguliwa na mlinda
mlango wa Azam Aishi Manula.
Kipre Tchetche, John Bocco,
‘Adebayor’, Himid Mao, Agrey Morris, Jean Mugiraneza, Erasto Nyoni na
Shomari Kapombe walifunga penati zao kwa upande wa Azam wakati Pascal
Wawa na Ame Ally ‘Zungu’ wao penati zao ziliokolewa na Ali Mustafa
‘Barthez’.
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni