JAJA SASA NATAKA KUWA MFUNGAJI BORA WA LIGI KUU
Mshambuliaji wa Yanga, Genilson Santana ‘Jaja’ amebainisha kuwa amepata nguvu mpya kuichezea Yanga na sasa anapiga hesabu ya kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu na kutwaa kiatu cha dhahabu. Jaja, ambaye hajui Kiswahili wala Kiingereza, aliliambia gazeti hili kupitia kwa mkalimani wake ambaye pia ni mchezaji wa Yanga, Andrew Coutinho anayezungumza Kiingereza na Kireno, kuwa sasa ameanza kupata amani kuichezea timu hiyo. “Mwanzo sikuwa na amani kabisa kutokana na mashabiki kutonikubali. Baada ya kufunga kwenye mechi yetu ya kirafiki na Thika United na leo (juzi) kufunga tena kwenye mechi na Azam, mashabiki wameanza kunipokea. “Sapoti yao inanipa matumaini na sasa ninachokifikiria ili niwafurahishe zaidi, ni kuhakikisha nafunga zaidi kwenye ligi na hatimaye kuwa mfungaji bora msimu huu,” alisema Jaja. Wakati huohuo, mashabiki wa Yanga wameutaka uongozi wa klabu hiyo kuachana na mchezaji, Emmanuel Okwi na kusisitiza kuwa Jaja amefiti kucheza nafasi hiyo. Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mashabiki hao walisema Jaja sasa ndiyo “habari ya mjini” na si Okwi, hivyo uongozi huo uachane naye kwani hana namba kwenye kikosi hicho cha Jangwani. “Nini Okwi, Jaja ndiyo habari ya mjini, tena bora tu hao viongozi waachane naye kwani kwenye kikosi cha Yanga hana nafasi ya kucheza,” alisema shabiki aliyejitambulisha kwa jina moja la Dennis.
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni