
LOUIS VAN GAAL yuko kwenye wakati mgumu baada ya Wachezaji wake Watatu wa Difensi kuwa Majeruhi na upo uwezekano mkubwa akalazimika kumtumia Kinda Paddy McNair wa Kikosi cha Vijana wa chini ya Miaka 21, U-21, kucheza Mechi ya Ligi Kuu England Uwanjani Old Trafford dhidi ya West Ham hapo Jumamosi.
Wakati Phil Jones na Jonny Evans wakiwa Majeruhi, Chris Smalling nae amepata tatizo la Mguu na ipo hatari kubwa asiweze kucheza Mechi hiyo ya Jumamosi.
Pamoja na hao, Chipukizi Tyler Blackett, ambae amekuwa akicheza Mechi zote 5 za Ligi Msimu huu, hataweza kucheza na West Ham baada ya Wikiendi iliyopita kulambwa Kadi Nyekundu wakati Man United inacheza na Leicester City.
Ingawa Kiungo Michael Carrick amepona Enka yake na huko nyuma ameshawahi kucheza Sentahafu ndani ya Man United, Mechi ya Jumamosi imekuja mapema kwake kwani ni Wiki iliyopita tu ndio alirejea Mazoezini baada ya kupona.
Taarifa toka ndani ya Old Trafford zimebainisha kuwa Van Gaal anatafakari kumtumia Paddy McNair, Kinda wa Miaka 19 kutoka Northern Island.
Tatizo hilo la Majeruhi wa Difensi ya Man United limeibua mjadala mkubwa kuhusu hekima ya kununua Wachezaji 6 wa Bei mbaya bila kuongeza hata Sentahafu mmoja, ukimwondoa Marcos Rojo ambae huweza kucheza Nafasi hiyo.
Vile vile, Man United huenda wakajuta kuhusu Beki wao Chipukizi, Michael Keane, mwenye Miaka 21 na ambae alicheza vizuri kwenye Ziara ya USA kabla Msimu kuanza, kukubali kumpeleka kwa Mkopo huko Burnley.
Mbali ya kumtumia Paddy McNair, Van Gaal inasemekana anafikiria kuwatumia Daley Blind na Marcos Rojo kama Masentahafu wakisaidiwa na Mafulbeki Rafael Da Silva na Luke Shaw, ambae ndio itakuwa Mechi yake ya kwanza akicheza.
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni