LOGO

KOCHA bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2009/2010, Patrick Phiri anatarajiwa kutua Dar es Salaam Ijumaa wiki hii kwa ajili ya kusaini Mkataba wa kuifundisha klabu yake ya zamani, Simba SC.
Mzaliwa huyo wa Mei 3 mwaka 1956, alifanya kazi kwa awamu tatu tofauti akiwa na Wekundu hao wa Msimbazi kati ya mwaka 2004 na 2010 na kwa mafanikio makubwa- na sasa anataka kurejesha enzi. Mzambia huyo alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu akiwa na Simba SC, misimu ya 2004/2005 na 2009/2010 na pia alishinda Makombe ya Tusker mwaka 2005 la Tanzania na Kenya.
 
Patrick Phiri
Mazungumzo yamekwishanyika na makubaliano yamefikiwa baina ya Phiri na Simba SC na sasa atakuja kufanya kazi tena Msimbazi, akisaidiwa na Nahodha wake enzi zake akifundisha timu hiyo, Suleiman Abdallah Matola ‘Osama’.

Phiri ni kocha anayekubalika zaidi mbele ya mashabiki wa Simba SC miongoni mwa makocha waliowahi kufundisha klabu hiyo- rekodi yake ya kukumbukwa zaidi ikiwa ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2009/2010 bila kufungwa hata mechi moja.

Lakini pia, namna alivyoweza kuiongoza Simba SC kuwatambia watani wa jadi, Yanga SC ni jambo lingine linalomfanya awe kocha mwenye heshima ya kipekee Msimbazi.

Katika awamu zote tatu alizofundisha Simba SC awali, Phiri hajawahi kufukuzwa- kwani amekuwa akiondoka mwenyewe kwa sababu mbalimbali. Kwa sasa, mume huyo wa Cecilia Mutale waliyezaa naye watoto wawili, Melesianiah na Patrick Junior, anarejea Simba SC akitokea Green Buffaloes ya Ligi Kuu ya Zambia.

Phiri ni kocha mwenye mafanikio tangu anacheza soka katika klabu za Rokana United (sasa Nkana F.C.) na Red Arrows zote za nyumbani kwao, Zambia kama mshambuliaji.

Alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zambia kilichocheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1978 na 1982, kabla ya kuiwezesha Chipolopolo kufuzu kwa AFCON ya mwaka 2008 nchini Ghana.
  Akiwa kocha, Phiri pia aliiongoza timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Zambia kucheza Fainali za kwanza kabisa za Kombe la Dunia nchini Nigeria mwaka 1997 kabla ya kushinda tuzo ya kocha bora wa mwaka nchini mwake mwaka 1999.

Simba SC jana ilivunja mkataba na Mcroatia, Zdravko Logarusic ikiwa ni siku moja tu baada ya timu hiyo kufungwa mabao 3-0 na ZESCO ya Zambia katika mchezo wa kirafiki juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Loga ambaye aliongezewa Mkataba wa mwaka mmoja mwezi uliopita- inadaiwa amefukuzwa kwa sababu za kutotii miiko na maadili ya klabu na Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva alisema jana kwamba uamuzi huo umekuja baada ya kumvumilia kwa kiasi cha kutosha.

Loga ameondoka Simba SC baada ya kuiongoza katika mechi 21 tangu Desemba mwaka jana, kati ya hizo akishinda nane, sare tano na kufungwa nane.
 
Loga aliyerithi mikoba ya Mzalendo, Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’, aliikuta Simba SC bado ipo kwenye mbio za ubingwa msimu uliopita, lakini mwishowe ikamaliza nafasi ya nne nyuma ya Mbeya City, Yanga SC na Azam FC mabingwa.
bin zubeiry

0 comments Blogger 0 Facebook

Chapisha Maoni

ZILIZOSOMWA SANA

 
TASWIRA MICHEZONI © 2015. All Rights Reserved. This Blog Proudly Designed by MMC™ Media Group Ltd | Phone +255-786-758-021
Top