Kauli ya Rais Kikwete imekuja wakati suala hilo
likionekana kuwagawa wajumbe katika Kamati za Bunge Maalumu, kutokana na
kuwapo kwa mapendekezo kwamba suala uraia pacha liingizwe kwenye rasimu
hata kama halikuwekwa na Tume.
Juzi, suala hilo liliwagawa wajumbe wa Kamati
Namba mbili inayoongozwa na Waziri Kiongozi mstaafu wa Zanzibar, Shamsi
Vuai Nahodha na kusababisha ibara hiyo kukosa theluthi mbili ya kura
kutoka pande zote za muungano.
Akizungumza katika kongamano maalumu
linalowakutanisha Watanzania waishio nje ya nchi Dar es Salaam jana,
Rais Kikwete alisema suala hilo limekosa wasemaji wanaoguswa moja kwa
moja ambao wangeweza kulitetea, hivyo kutokuwa miongoni mwa vipaumbele
katika rasimu hiyo.
“Msijipe matumaini kwa sababu kwa namna
ilivyoandikwa kwenye Rasimu ya Katiba, haiwezi kuzaa uraia wa nchi
mbili, bali inaweza kutoa stahiki ya fursa wanazoweza kupata Watanzania
waishio nje ya nchi, kupitia sheria,” alisema.
Kongamano hilo la kwanza la siku mbili
linawakutanisha Watanzania waishio katika nchi 17 duniani,
lililoandaliwa na Asasi ya Tanzania Diaspora Initiative (TDI).
Rais Kikwete alisema Serikali yake inafahamu
umuhimu wa kupatikana kwa uraia pacha kwa watu wake lakini suala la
uraia ni la kikatiba na siyo la Rais kwa kuwa Katiba ndiyo inayoamua.
Alisema hata chama chake (CCM), kilipojaribu
kuliingiza lilionekana kutokuwa na nguvu ya kutosha kwa kuwa hakuna
ambaye lilikuwa likimgusa moja kwa moja.
Aliwashauri kuwatumia wajumbe katika Bunge
linaloendelea mjini Dodoma ili wapaze sauti zao na ikiwezekana watumie
fursa zote za mawasiliano kufikisha ujumbe wao.
“Sisi upande wa Serikali tunaliona ni suala jema,
ila halina nguvu kwa sababu wabunge wengi haliwagusi moja kwa moja,
hivyo si rahisi kulipigania. Mbona nchi nyingine watu wao wananufaika na
hili! Kwa nini hapa kwetu lishindikane?” alihoji.
Ndani ya kamati
Habari kutoka ndani ya kamati zinasema wajumbe
wamegawanyika kuhusu suala hilo na wengine wameshindwa kufikia mwafaka
kama ilivyotokea katika Kamati namba 11 inayoongozwa na Mbunge wa Same
Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni