LOGO

BEKI Shomary Kapombe na mshambuliaji Lionel Saint- Preux kutoka Haiti wote wamefanya mazoezi kikamilifu jana na leo kuelekea mchezo wa kesho wa Robo Fainali Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Azam FC ikimenyana na El Marreikh ya Sudan, Uwanja wa Nyamirambo, Kigali, Rwanda.
Wawili hao waliokuwa wanasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja, walikoa mchezo wa mwisho wa Kundi A dhidi ya Adama City ya Ethiopia, Azam FC ikishinda 4-1.

Na katika mazoezi ya leo asubuhi Uwanja wa Kiyovu, Nyamirambo mjini hapa, kocha Mcameroon Joseph Marious Omog ameonekana kuwahusisha nyota hao katika kikosi kitakachoanza kesho.
Majeruhi mwingine, beki Waziri Salum pia amefanya mazoezi wakati kiungo Himid Mao anatarajiwa kurudi pia baada ya kukosa mchezo dhidi ya Adama kwa sababu ya kadi za njano.
Omog amekuwa akiandaa Azam FC kitaalamu mno kuelekea mchezo huo, akiwaelekeza mifumo na aina tofauti ya uchezaji, ikiwa ni pamoja na kutumia mipira mirefu na mifupi.
Amekuwa akiwandaa pia kwa kupiga penalti, kwa kuwa iwapo mchezo huo utamalizika kwa sare, matuta yataamua timu ya kusonga Nusu Fainali.
Kwa ujumla Azam ambayo imewekwa hoteli moja na wapinzani wao hao, Merreikh, Kigali View eneo la Nyamirambo, ipo vizuri kuelekea mchezo huo, ambao unasubiriwa kwa hamu na Watanzania wengi.
Robo Fainali za Kagame zinaanza leo, mchezo wa kwanza ukiwa kati ya Polisi ya hapa dhidi ya Atleitco ya Burundi, kabla ya Rayon Sport kumenyana na APR, zote za hapa leo, wakati mbali na Azam na Merreikh, mchezo mwingine wa kesho utakuwa kati ya KCC ya Uganda na Atlabara ya Sudan Kusini.

0 comments Blogger 0 Facebook

Chapisha Maoni

ZILIZOSOMWA SANA

 
TASWIRA MICHEZONI © 2015. All Rights Reserved. This Blog Proudly Designed by MMC™ Media Group Ltd | Phone +255-786-758-021
Top