KOCHA Mkuu wa Azam FC, Joseph Marius Omog amesema kwamba kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Omog amesema japokuwa atamkosa Nahodha wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’, lakini anaamini wachezaji waliobaki wana uwezo wa kuiwezesha Azam FC kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya kwanza kesho.
“Tuko tayari, vijana wapo katika hali nzuri kuelekea mchezo huo muhimu wa mwanzo wa msimu. Nitamkosa Nahodha John (Bocco), lakini nina imani kubwa na wachezaji waliopo,”amesema Mcameroon huyo.
John Bocco anasumbuliwa na maumivu ya nyama aliyoyapata katika mchezo wa Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita Kigali, Rwanda.
Akiwazungumzia wapinzani, Omog amesema kwamba anaiheshimu Yanga SC ni timu kongwe na yenye historia katika soka ya Tanzania na anatarajia mchezo wa kesho utakuwa mgumu, lakini wamejiandaa kikamilifu kushinda.
Timu hizo za Dar es Salaam zitakutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo kesho Uwanja wa Taifa, baada ya mwaka jana Yanga kuifunga Azam FC bao 1-0.
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni