TFF YARIDHIA MANJI KUONGEZEWA MUDA UENYEKITI YANGA SC
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limebariki mwenyekiti ya Yanga, Yusuf Manji kuongezewa muda baada ya kushindwa kulifikisha suala la katiba ya klabu hiyo kwa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji. Awali TFF ilikuwa ikipigia kelele Yanga iwasilishe muhtasari wake wa mkutano mkuu uliofanyia marekebisho katiba Juni Mosi mwaka huu, lakini tangu Yanga ilipopeleka yapata mwezi mmoja sasa, TFF imegeuka bubu kuhusu katiba hiyo. Kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji chini ya Mwanasheria Richard Sinamtwa kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, kilipaswa kupitia masuala mbalimbali ya usajili ikiwemo kuipitia katiba hiyo ili kuangalia kama inaendana na ile ya TFF kabla ya kupelekwa kwa msajili wa vyama vya michezo na kwenda kwenye uchaguzi mkuu. Habari ambazo gazeti hili limezipata ni kuwa TFF wamebariki Manji kuendelea kuongoza mwaka mmoja kama mkutano mkuu ulivyoazimia. “Kwa kawaida Kamati ya Sheria ilipaswa ipitie na kuangalia kama ina upungufu, kama haina ipitishe, lakini TFF hawakuipeleka ajenda hiyo hivyo kamati haikujadili. “Nilitegemea kama TFF wataipeleka kama ajenda basi itajadiliwa kwenye dirisha dogo, wasipoipeleka ndiyo imetoka, labda baadaye waitishe tena kikao cha dharura ni gharama,” alisema mpashaji wetu. Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Moses Karua alisema jana kwa kifupi “TFF hawakutuletea ajenda hiyo ya katiba, labda wenyewe wanajua ‘watahandle’ vipi suala hilo. Labda watalimalizia kwenye ngazi za sekretarieti.” Katibu mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema: “Bado tunalifanyia kazi.” Gazeti hili lilipotaka kufahamu zaidi kwa nini katiba hiyo haikupelekwa kama ajenda kwenye kikao hicho, alisema: “Wewe jua TFF inafanyia kazi, kufanyiwa kazi siyo lazima ijadiliwe na Kamati ya Sheria.”
MWANANCHI
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni