Kocha wa Yanga, Marcio Maximo amejigamba kuwa kikosi chake kipo tayari kila idara kwa Ligi Kuu Bara, lakini mwenzake Patrick Phiri wa Simba ana kazi ya kuimarisha ubora katika safu yake ya ulinzi.
Mabingwa wa Ngao ya Jamii wataanza kampeni ya
kusaka ubingwa wa Bara kwa kuivaa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri,
Morogoro Jumamosi wiki hii.
Rekodi zinambeba zaidi Maximo kwani katika mechi
tano alizoiongoza Yanga, hajashindwa wala kuruhusu bao lolote langoni
kwake huku Simba ikipoteza mechi moja na kutoka sare moja.
Yanga chini ya Maximo ilianza na ushindi wa bao
1-0 dhidi ya Chipukizi ya Pemba, bao lililofungwa na Genilson Santos
‘Jaja’, baadaye ikaifunga Shangani mabao 2-0 wafungaji wakiwa Andrey
Coutinho na Salum Telela. Yanga pia iliilaza KMKM mabao 2-0 wafungaji
wakiwa Coutinho na Hussein Javu kabla ya Jaja kufunga bao pekee wakati
Yanga ilipoilaza Thika United ya Kenya. Yanga ilimalizia kwa ushindi
mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Azam FC mwishoni mwa wiki katika mechi ya
Ngao ya Jamii, Jaja akitikisa mabao mawili na jingine likifungwa na
Simon Msuva.
Simba imecheza mechi sita na kushinda nne, imetoka
sare moja na kufungwa moja. Simba ilizifunga Kilimani 2-1 kwa mabao ya
Haruna Chanongo na Shaaban Kisiga, baadaye ikaifunga Mafunzo 2-0
(Chanongo na Elius Maguli) kabla ya kuitandika KMKM mabao 5-0
yaliyofungwa na Amissi Tambwe (mawili), Maguli, Kisiga na Amri Kiemba.
Baadaye Simba iliifunga Gor Mahia mabao 3-0
(Raphael Kiongera (mawili) na Ramadhan Singano), lakini ikachapwa bao
1-0 na URA ya Uganda na kumaliza kwa kwenda suluhu na Ndanda FC ya
Mtwara kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Pamoja na rekodi hiyo kumbeba Maximo, kauli yake ya kutambia kikosi chake pia imekuja baada ya kuifunga Azam FC mabao 3-0.
Akizungumza na gazeti hili, Maximo alisema kikosi
chake kimeonyesha mwanga wa kufanya vizuri msimu ujao kwani kila mtu
anawajibika ipasavyo kwenye nafasi yake.
“Hapa unaweza kuona tumeshinda mchezo huu kwa kuwa
kila idara inafanya kazi yake. Sisi watu wa benchi la ufundi tunafanya
kazi kwa kushirikiana kwa karibu mno. Wasaidizi wangu kuanzia Neiva
(Leonadro), Salvatory (Edward) na Shadrack (Nsajigwa) wote
tunasilikizana,” alisema Maximo.
“Hata ukitazama wachezaji utagundua wote wana
uwezo wa kucheza kikosi cha kwanza hivyo tena kwa mtindo tofauti tofauti
ndiyo maana unaweza kuona anatoka fulani anaingia mwenzake ambaye
anafanya vizuri pia.
“Ukiachana na mtindo tofauti hata uwezo wa
wachezaji nao siyo wa aina moja hivyo wapo wachezaji watakaocheza aina
fulani ya mechi kwa ajili ya matokeo fulani. Kwa jumla Yanga ina kikosi
imara ambacho sasa kipo tayari kwa mapambano japokuwa kuna vitu vidogo
vya kurekebisha,” alisema Maximo.
Kauli hiyo ya Maximo inachagizwa na kitendo cha
Yanga kucheza mechi tano na kushinda zote huku ikiwa haijaruhusu hata
bao moja katika nyavu zake na kupata mabao tisa huku straika Genilson
Santos ‘Jaja’ akiongoza kwa kufunga mabao manne.
MWANANCHI
MWANANCHI
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni