LOGO

YANGA SC imeshinda mechi ya pili mfululizo katika ziara yake ya Zanzibar baada ya kuichapa mabao 2-0 Shangani ya Daraja la Pili Wilaya ya Mjini, mkoa Mjini Magharibi Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Yanga SC juzi iliifunga bao 1-0 Chipukizi ya Pemba Uwanja wa Gombani, bao pekee la Geilson Santana ‘Jaja’ na leo imetua kisiwani Unguja kuendeleza adhabu. 
Hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Mbrazil, Andrey Coutinho dakika ya saba kwa shuti la umbali wa mita 18 baada ya kupokea pasi ya Hassan Dilunga na kuwahadaa wachezaji wawili wa Shangani.
Coutinho alifurahi mno kufunga bao lake la kwanza Yanga SC na kwenda kushangilia mbele ya mashabiki kabla ya kupiga magoti na kusali.
Mshambuliaji pekee katika mfumo wa Maximo, Geilson Santana ‘Jaja’ leo alishindwa kufurukuta mbele ya safu ya ulinzi ya vijana wadogo wa Shangani, wakati Coutinho alikuwa mwiba haswa.
Kocha Maximo alibadilisha timu nzima kipindi cha pili, kasoro Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Kiungo ambaye kwa sasa anachezeshwa beki ya kulia, Salum Abdul Telela ‘Master’ aliifungia Yanga SC bao la pili dakika ya 59. 
Viongozi wa Simba wakiongozwa na Makamu wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, Kassim Dewji, Mohammed Nassor ‘Steven Seagal’, Collins Frisch, na Iddi Kajuna walikuwepo jukwaani kuwashuhudia wapinzani wao hao wa jadi, ambao watakutana nao katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Oktoba 12, mwaka huu.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’/Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul/Salum Telela, Oscar Joshua/Amos Abel, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan/Rajab Zahir, Mbuyu Twite/Omega Seme, Haruna Niyonzima/Hamisi Kiiza, Hassan Dilunga/Hamisi Thabit, Geilson Santana ‘Jaja’/Jerry Tegete/Said Bahanuzi dk70, Simon Msuva/Hussein Javu na Andrey Coutinho/Nizar Khalfan. 
Shangani; Hasham Haroun, Hussein Kilahe, Iddi Hussein, Omar Mahmoud, Seif Maulid, Mussa Mbarouk, Ismail Kassim/Ali Makame Fumu dk70, Adam Ibrahim, Hassan Kilahe,  Mohammed Pandu na Abrahman Mbarouk/Khamis Bakari dk55.

bin zubeiry

0 comments Blogger 0 Facebook

Chapisha Maoni

ZILIZOSOMWA SANA

 
TASWIRA MICHEZONI © 2015. All Rights Reserved. This Blog Proudly Designed by MMC™ Media Group Ltd | Phone +255-786-758-021
Top