LOGO



Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Leodegar Tenga.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Leodegar Tenga, amesema hatua ya Yanga kutoshiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) mwaka huu ni sawa na 'kujimaliza' yenyewe na kwamba haitaadhibiwa tena.
Yanga haitapata adhabu yoyote ya kufungiwa na Cecafa baada ya awali kuondolewa katika mashindano hayo kutokana kuleta kikosi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Azam ya Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini Kigali Rwanda, Tenga, alisema Yanga imekosa fursa ya kutumia nafasi muhimu ya kuimarisha kikosi chake kiufundi na vile vile kujitangaza ili kupata wadhamini watakaoisaidia kuiendesha.

Tenga alisema mashindano hayo yameandaliwa maalumu kwa ajili ya kuwaandaa mabingwa na michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ligi za nchi zao, hivyo kuleta timu ya vijana ni kukiuka kanuni za michuano.

Alisema Yanga imepoteza nafasi ya kujitangaza kwa sababu makampuni yote hutoa fedha pale inapoona timu inashiriki kwenye mashindano ya kimataifa hivyo nao watafaidika kwa kutangazwa.

"Kuwaondoa Yanga kushiriki hatukuwaonea, kanuni zilifuatwa. Ni lazima kila mmoja aheshimu kanuni, mwanachama ambaye haheshimu kanuni hatutamruhusu na badala yake tutamuacha aendelee na mambo mengine," Tenga alisema. "Haya mashindano ni kwa ajili ya kuwaona mabingwa kuonyesha viwango vyao na ni sehemu pia ya kujitangaza kibiashara."

Rais huyo wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),  alisema Cecafa imefurahishwa na viwango vya timu zote 14 zilizoshiriki mashindano ya mwaka huu kwa kuonyesha ushindani kuanzia hatua ya makundi.

Aliongeza kuwa unapoona hatua ya robo fainali, mechi tatu zinaamuliwa kwa penalti, basi timu ni bora na malengo ya kukuza soka kwenye ukanda huu yameanza kuonekana.

Kadhalika, alimshukuru Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kwa kuendelea kudhamini michuano hiyo ya kila mwaka pamoja na wadau wote wa soka kwenye ukanda huu kwa ushiriki wao.

"Kila mwaka Rais, Paul Kagame, amekuwa kimbilio letu, kila tunapokwama yeye amekuwa akiokoa mashindano, pia kwa wananchi wa Rwanda kujitokeza kushuhudia mechi. Tunashuruku mashindano yamefanyika kwa mafanikio tofauti na ilivyokuwa mwaka jana nchini Kenya (Kombe la Chalenji) hali haikuwa nzuri," aliongeza Tenga.

Alisema maandalizi sahihi ya timu yoyote yanapatikana katika kushiriki kwenye mashindano na si vinginevyo.

Yanga ilikataa kupeleka wachezaji wake wa kikosi cha kwanza katika mashindano hayo na kuamua kuchagua Kikosi B na wachezaji wa umri chini ya miaka 20 huku ikitangaza Kikosi A na Kocha Mkuu, Mbrazil, Marcio Maximo, kwenda Pemba kuweka kambi kujiandaa na Ligi Kuu ya Bara.

Nchi itakayoandaa michuano hiyo mwakani itajulikana baadaye Novemba mwaka huu katika Mkutano Mkuu wa Cekafa wa mwaka utakaofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia.

0 comments Blogger 0 Facebook

Chapisha Maoni

ZILIZOSOMWA SANA

 
TASWIRA MICHEZONI © 2015. All Rights Reserved. This Blog Proudly Designed by MMC™ Media Group Ltd | Phone +255-786-758-021
Top