LOGO

Wakati kiungo mpya wa Yanga kutoka Brazil, Andrey Coutinho akirejea mazoezini, kikosi cha Wanajangwani hao kinatarajiwa kutua mjini Morogoro leo kwa ajili ya mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini humo Jumamosi.
Coutinho alipata majeraha ya kifundo cha mguu wakati wa mechi ya mazoezini waliyotoka suluhu na timu ya Polisi Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola wiki iliyopita, majeraha ambayo yalisababisha aikose mechi ya Ngao ya Jamii waliyoshinda 3-0 dhidi ya Azam FC Jumapili.
Jana asubuhi NIPASHE ilimshuhudia kiungo huyo aliyeteka vichwa vya magazeti ya michezo nchini akifanya mazoezi na wachezaji wengine wa Yanga kwenye uwanja wa shule hiyo kujiandaa kwa mechi inayofuata dhidi ya Mtibwa.
Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kuwa, kikosi chao kinachonolewa na kocha wa zamani wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbrazil Marcio Maximo kinatarajia kusafiri kwenda Morogoro leo kumenyana na wakatamiwa hao wa Manungu, Turiani.
"Tumepanga timu iende Morogoro kesho (leo) au keshokutwa (Ijumaa). Tunashindwa kuamua moja kwa moja siku ya kwenda huko kwa sababu tunaambiwa uwanja umepangwa kutumika kwa shughuli za burudani," alisema Njovu.
Yanga, mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara na mara tano wa Kombe la Kagame, watakuwa na mtihani mgumu mbele ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri ambao kikosi cha nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Mexime hakijawahi kufungwa na Yanga tangu Septemba 19, 2009 kwenye uwanja huo.
Kikiwa chini ya kocha Mserbia, Profesa Dusan Kondic, kikosi cha Yanga kilipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Mtibwa. Mabao yakifungwa na wachezaji wa mwisho kuipa Yanga ushindi kwenye uwanja huo, Nurdin Bakari aliyefunga dakika ya 55 na Mrisho Ngasa dakika ya 57.
Tayari Mexime ameshaweka wazi kwamba anazifahamu kwa undani mbinu za Maximo kwa vile aliwahi kumfundisha akiwa nahodha wa Taifa Stars, hivyo ana kazi nyepesi kuhakikisha anaifunga tena Yanga ambayo haijawahi kufungwa hata bao moja tangu ianze kunolewa na Mbrazil huyo.
Mtibwa Sugar iliyoanzishwa 1988 na kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara mara mbili mfululizo 1999 na mwaka wa mabadiliko ya karne, imekuwa ikionesha upinzani mkali kwa klabu kongwe na zenye mashabiki lukuki nchini, Simba na Yanga, hasa zinapokwenda kucheza dhidi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Msimu uliopita wa VPL, Mtibwa ilizilazimisha sare timu hizo kwenye uwanja huo na kuharibu harakati za Yanga kutetea taji lake la VPL lililotwaliwa na Azam FC.
Yanga, mbali na kupotezwa maboya na Mtibwa katika mbio za ubingwa msimu uliopita, itaingia kwenye Uwanja wa Jamhuri ikiwa na kumbukumbu ya kupokea kichapo kikali cha mabao 3-0 kutoka kwa timu hiyo msimu wa 2012/13, kipigo kilichosababisha kutimuliwa kwa aliyekuwa kocha mkuu Mbelgiji Tom Saintfiet.



NIPASHE

0 comments Blogger 0 Facebook

Chapisha Maoni

ZILIZOSOMWA SANA

 
TASWIRA MICHEZONI © 2015. All Rights Reserved. This Blog Proudly Designed by MMC™ Media Group Ltd | Phone +255-786-758-021
Top