Beki wa kati na nahodha wa Yanga, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, ameshangazwa na kitendo cha kiungo mshambuliaji wa timu hiyo,
Mganda, Emmanuel Okwi kusaini Simba huku akimwambia: “Tutaonana uwanjani.”
Aliongeza kuwa, hasikitiki na haogopi hata
kidogo kuondoka kwa kiungo huyo huku akimtamkia kwamba watajuana vizuri mara
watakapokutana uwanjani kama akifanikiwa kuichezea Simba.
“Ujue nilishangaa na kushtushwa juu ya Okwi
kusaini mkataba wa kuichezea Simba, ninaona kama filamu ya maigizo kwa kiungo
huyo kusaini mkataba akiwa ana mkataba mwingine.
“Nafikiri huyo mchezaji anataka uwe mwisho
wake wa kucheza soka, ni maamuzi magumu ameyachukua, lakini katika hilo sitaki
niliongelee sana, kikubwa nitaonana na mchezaji huyo ndani ya uwanja mara
tutakapokutana,” alisema Cannavaro.
Wakati Cannavaro akisema hayo, Okwi mwenyewe amewaahidi
ubingwa wa Ligi Kuu Bara mashabiki wa Simba.
“Ninajua mashabiki wa Simba wana kiu ya
ubingwa wa ligi kuu, hivyo waondoe hofu mara baada ya kurejea kwenye klabu
niipendayo kutoka moyoni.
“Niliichezea Yanga kwa maslahi, lakini siyo
mapenzi kutoka moyoni, hivyo mashabiki watarajie mengi kutoka kwangu,” alisema
Okwi.
0 comments Blogger 0 Facebook
Chapisha Maoni